Update:

De Gea kusaini mkataba mpya Man United ?


  Ikiwa imepita wiki moja tangu usajili wake kuelekea klabu ya Real Madrid kushindikana kwenye dakika za mwisho za dirisha la usajili , kipa wa Manchester United David De Gea amenukuliwa akisema anahisi anawajibika kusaini mkataba mpya ndani ya klabu hiyo .

De Gea mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akisakwa kwa udi na uvumba na Real Madrid ambao kwenye dakika za mwisho za dirisha la usajili waliongeza kasi ya kutaka kumsajili kwa kukubali kuilipa Manchester United ada ya uhamisho ya paundi milioni 29 pamoja na kumruhusu kipa Keylor Navas kujiunga na klabu hiyo .

Usajili huo hata hivyo ulifeli baada ya kucheleweshwa huku pande zote mbili zikilaumu upande mwingine kwa kuchelewesha nyaaka muhimu .

De Gea amenukuliwa na gazeti la kila siku nchini England la Metro akisema kuwa anahisi kwamba kwa sasa anapaswa kusaini mkataba mpya kwani bila kufanya hivyo hatopata nafasi kwenye kikosi cha kwanza .

Kocha wa United Mdachi Louis Van Gaal hadi sasa amekuwa mzito kumpanga De Gea kwenye michezo ya ligi kuu na ligi ya mabingwa kutokana na suala lake la usajili lakini baada ya usajili huo kushindikana Van Gaal amesema yuko tayari kumrudisha De Gea kundini .

Kumekuwa na tetesi kadhaa zikidai kuwa De Gea atajiunga na Madrid kwenye dirisha dogo la usajili mwezi januari lakini uongozi wa United umeendelea kushikilia msimamo wake ukisema kuwa mchezaji huyo hatauzwa januari .

Wengi wanashawishika kuamini kuwa De Gea hatasaini mkataba mpya na badala yake atangoja mpaka kumalizika kwa mkataba wake wa sasa ambayo umebakiza mwaka mmoja na kujiunga na Real Madrid bure msimu ujao .